chakarika

Tuesday 12 October 2010

Bado tumejifunga katika mantiki iliyopinda





Jenerali Ulimwengu Oktoba 6, 2010


SIKU zinazidi kuyoyoma, na uchaguzi uliosubiriwa na wengi unazidi kukaribia. Hamasa zinazidi kupamba moto na shauku za washiriki wa kila aina zinazidi kujidhihirisha.

Kama ilivyo kote katika bara letu, Afrika, uchaguzi unabeba umuhimu ambao haupatikani katika nchi za wenzetu walioendelea. Kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea, kipindi cha uchaguzi ni kipindi cha kujipima nguvu kwa mara nyingine na kushindanisha sera na kuomba ridhaa ya wananchi wakubali kuongozwa na mmoja wa washindani.

Hakuna vita, hata kama wakati mwingine maneno yanakuwa makali na wanasiasa watabeza na kukejeli washindani wao. Ni mara chche sana itasikika kwamba wafuasi wa chama kimoja wamepigana na kutoana ngeu na wafuasi wa chama kingine, au kusikia kwamba jeshi la polisi limefyatua risasi na kuwajeruhi wafuasi wa cha fulani.

Mambo yanakuwa shwari, kampeni zinaendeshwa kwa amani, na kura zinapigwa katika utulivu, na ingawaje imewahi kutokea kukawa na ubishani kuhusu matokeo (kama baina ya Joji W. na Al Gore) si kawaida kusikia malalamiko kuhusu hilo.

Kimsingi hali hii inatokea katika nchi za wenzetu kwa sababu uchaguzi, ingawa ni muhimu, si suala la kufa na kupona. Watu hushiriki katika kampeni kwa nguvu zao zote, wakalumbana kwa hoja zilizopangiliwa vyema, wakacheza dansi, wakaimba, wakafanya matamasha kila mahali wakiburudika, kisha wakapiga kura. Wanaoshinda wanapongezana, na wanaoshindwa wanaliwazana. Kisha wote wanarejea katika shughuli zao za kawaida.

Hawa wana shughuli zao za kuwapa riziki, na ambazo ndizo muhimu kuliko uchaguzi ambao kwao ni zoezi la msimu. Wanarudi katika uzalishaji na utoaji huduma hadi kipindi kingine cha uchaguzi kitakapowadia.

Afrika ni tofauti kabisa. Kila uchaguzi unachukuliwa kama vita, ni suala la kufa na kupona. Tofauti na hali ya wenzetu niliowaeleza hapo juu, washiriki wengi katika michakato ya uchaguzi katika nchi za Afrika hawana shughuli yo yote nyingine ya kufanya. Hawamo katika uzalishaji wala utoaji huduma; hawana ajira.

Aidha, katika nchi takriban zote za Afrika, uchaguzi ndio unaamua ni akina nani ‘watakula’ kwa kipindi chote hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika, na akina nani watanyimwa ‘mlo’ kwa kipindi chote hicho, kwa maana ya kwamba anayeshinda anashinda na kuchukua kila kitu na anayeshindwa anapoteza kila kitu, siyo yeye mwenyewe pekee bali pia ndugu, jamaa, marafiki na washirika wake wote.

Ushindi katika uchaguzi wa Kiafrika hufungua milango ya neema kubwa kwa mshindi na washirika wake. Kinara wa ushindi huo, ambaye mara nyingi huitwa ‘rais’, anakuwa ndiye kisima cha kila kitu: mamlaka ya dola; uwezo wa kumfanya ye yote asiye kitu kuwa mtu; uwezo wa kufikiri kuliko mtu ye yote mwingine; ukwasi na utajiri usiotokana na juhudi ya uzalishaji wala biashara; tunu ya kuwa na wanafamilia wanaojitokeza ghafla kuwa wenye akili na uwezo mkubwa, na kadhalika.

Yule anayeshindwa, hali yake ni mbaya sana, kwani kushinda si kupoteza uchaguzi tu na fursa ya kutoa mchango katika kuisaidia jamii kuendelea; ni zaidi ya hilo. Kwanza aliyeshindwa huonekana kama mkorofi, kwa sababu tu alithubutu kushindana na yule aliyeshinda.

Namna gani yule anayekuja kushindwa anaweza kujua nani atashinda tangu mwanzo ili asimpinge akaonekana mkorofi baada ya kuwa ameshindwa? Hili ni swali gumu, lakini mantiki ya siasa za Waafrika ni kwamba aliyeshindwa ndiye mkorofi, ndiye mwenye uchu wa madaraka, ndiye anayewagawa wananchi na ndiye mwenye kutaka kuleta vurugu nchini. Hiyo ndiyo mantiki iliyopinda ya Waafrika wengi walio madarakani.

Lakini ukorofi wa yule ambaye hatimaye atashindwa hudhihirika pale ambapo huyo mshindani mkorofi anapompinga aliye madarakani, ndiyo kusema yupo mtawala madarakani, na anaendesha serikali yake vizuri tu, naye anaamini kwamba kazi yake anaifanya kama anavyotakiwa, halafu anajitokeza mtu mwingine kusema anataka jukumu la kuongoza nchi akabidhiwe yeye.

Katika mantiki ya siasa za Kiafrika, ni dhahiri kwamba huyu anayeibuka kusema anataka kumwondoa mtu aliye madarakani ndiye mkorofi, kwa sababu kazi anyoitaka ina mtu tayari, na mtu huyo anaifanya vizuri tu. Haionekani sababu ya mtu mwingine kutaka kuchukua kazi ambayo tayari ina mtu na mtu anaifanya vizuri isipokuwa mkorofi tu.

Kabla hajashindwa mkorofi huyo atafanyiwa kila aina ya vituko ili kumsaidia kuelewa kwamba anachojaribu kukifanya hakiingiii akilini. Atafuatwafuatwa na mawakala wa vyombo vya dola; atasongwasongwa ili asijisikie huru na mwenye nafasi ya kutenda; atapelekewa maneno ya kumtisha na kumkatisha tamaa; atachunguzwa na asasi zinazohusika na kodi au jinai; atadodoswa kuhusu maisha yake binafsi; atachokonolewa kama vile ni nyoka na watu wanataka kuona miguu yake....

Kila juhudi zitafanywa ili kumzuia na labda kumfanya aache dhamira yake ya kutaka kuchukua kazi ambayo tayari inayo mtu na mtu huyo anaifanya vizuri. Baada ya vitisho na kila aina ya hekaheka na uchaguzi ukafanyika, huyo mkorofi akishinda wale walio madarakani wanaweza wakaukataa ushindi huo, wakaufuta. Wanaweza kufanya hivyo kwa sababu uwezo wanao, majeshi wanayo na asasi za utawala zote wanazo.

Imetokea mara kadhaa katika nchi za Kiafrika kwamba wananchi wanapiga kura kumchagua mtu fulani au chama fulani, lakini waliomo madarakani wanakataa, tena kwa nyuso kavu kabisa, kuachia madaraka.

Katika nchi kama hizo, wale waliopigiwa kura na wananchi lakini wakapokonywa ushindi ndio wanaoonekana kama wakorofi, hasa kama wananchi waliokasirishwa na udhalimu wataasi. Waliobiwa ndio wanakuwa watuhumiwa wakuu, na watuhumu wao ni wale waliowaibia.

Sitaki kusema kwamba kila mara walioshindwa wanakuwa wameibiwa, la hasha. Hutokea kwamba walioshindwa wameshindwa kweli, lakini zahama wanazozipata bado ni zile zinazoashiria kwamba ni wakorofi na wavurugaji kwa sababu tu walidiriki kutaka kuchukua nafasi isiyokuwa yao. Watapatilizwa kwa kosa hilo ambalo limeruhusiwa na katiba ya nchi.

Haya si ya kutunga, haya si ya kuzua, mifano tunayo tele. Ukweli ni kwamba Waafrika wengi bado hawajakubali msingi wa siasa za ushindani, bado. Bado tuko katika enzi za ‘mwenye nguvu mpishe’ na hapa nguvu ina maana nguvu za mabavu ya vyombo vya dola, au nguvu za mabavu mbadala, kwani wale wanaohisi wameonewa wanaweza pia kujenga uwezo wao wa kimabavu.

Kwa jinsi hii Waafrika tunajidumaza, hatuendi ko kote. Haishangazi, basi, kwamba baada ya nusu karne ya Uhuru na utawala wetu wenyewe, umasikini unazidi kukua, adha zinazidi kutuandama na ghadhabu za wananchi zinazidi kupanda. Sijui kama watawala wetu wanaliona hilo, na kama wanaliona sijui kama wanaamini kwamba njia ya kukabiliana nalo ni kutoa matamshi ya kutishana.

Matamko ya hivi karibuni kutoka kwa vyombo vilivyo karibu mno na utawala yanatia shaka kwamba watawala wanataka kuwafanya wananchi waamini kwamba wale wanaowapinga ni wakorofi na wachokozi. Inatia hofu kwamba labda na sisi hatujaondokana na mantiki niliyoieleza hapo juu. Matamko haya hayafai kwa sababu ni ya hatari.

Tunahitaji kufanya hadhari kubwa ili kuepusha janga kuu.