chakarika

Tuesday 12 October 2010

Bado tumejifunga katika mantiki iliyopinda





Jenerali Ulimwengu Oktoba 6, 2010


SIKU zinazidi kuyoyoma, na uchaguzi uliosubiriwa na wengi unazidi kukaribia. Hamasa zinazidi kupamba moto na shauku za washiriki wa kila aina zinazidi kujidhihirisha.

Kama ilivyo kote katika bara letu, Afrika, uchaguzi unabeba umuhimu ambao haupatikani katika nchi za wenzetu walioendelea. Kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea, kipindi cha uchaguzi ni kipindi cha kujipima nguvu kwa mara nyingine na kushindanisha sera na kuomba ridhaa ya wananchi wakubali kuongozwa na mmoja wa washindani.

Hakuna vita, hata kama wakati mwingine maneno yanakuwa makali na wanasiasa watabeza na kukejeli washindani wao. Ni mara chche sana itasikika kwamba wafuasi wa chama kimoja wamepigana na kutoana ngeu na wafuasi wa chama kingine, au kusikia kwamba jeshi la polisi limefyatua risasi na kuwajeruhi wafuasi wa cha fulani.

Mambo yanakuwa shwari, kampeni zinaendeshwa kwa amani, na kura zinapigwa katika utulivu, na ingawaje imewahi kutokea kukawa na ubishani kuhusu matokeo (kama baina ya Joji W. na Al Gore) si kawaida kusikia malalamiko kuhusu hilo.

Kimsingi hali hii inatokea katika nchi za wenzetu kwa sababu uchaguzi, ingawa ni muhimu, si suala la kufa na kupona. Watu hushiriki katika kampeni kwa nguvu zao zote, wakalumbana kwa hoja zilizopangiliwa vyema, wakacheza dansi, wakaimba, wakafanya matamasha kila mahali wakiburudika, kisha wakapiga kura. Wanaoshinda wanapongezana, na wanaoshindwa wanaliwazana. Kisha wote wanarejea katika shughuli zao za kawaida.

Hawa wana shughuli zao za kuwapa riziki, na ambazo ndizo muhimu kuliko uchaguzi ambao kwao ni zoezi la msimu. Wanarudi katika uzalishaji na utoaji huduma hadi kipindi kingine cha uchaguzi kitakapowadia.

Afrika ni tofauti kabisa. Kila uchaguzi unachukuliwa kama vita, ni suala la kufa na kupona. Tofauti na hali ya wenzetu niliowaeleza hapo juu, washiriki wengi katika michakato ya uchaguzi katika nchi za Afrika hawana shughuli yo yote nyingine ya kufanya. Hawamo katika uzalishaji wala utoaji huduma; hawana ajira.

Aidha, katika nchi takriban zote za Afrika, uchaguzi ndio unaamua ni akina nani ‘watakula’ kwa kipindi chote hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika, na akina nani watanyimwa ‘mlo’ kwa kipindi chote hicho, kwa maana ya kwamba anayeshinda anashinda na kuchukua kila kitu na anayeshindwa anapoteza kila kitu, siyo yeye mwenyewe pekee bali pia ndugu, jamaa, marafiki na washirika wake wote.

Ushindi katika uchaguzi wa Kiafrika hufungua milango ya neema kubwa kwa mshindi na washirika wake. Kinara wa ushindi huo, ambaye mara nyingi huitwa ‘rais’, anakuwa ndiye kisima cha kila kitu: mamlaka ya dola; uwezo wa kumfanya ye yote asiye kitu kuwa mtu; uwezo wa kufikiri kuliko mtu ye yote mwingine; ukwasi na utajiri usiotokana na juhudi ya uzalishaji wala biashara; tunu ya kuwa na wanafamilia wanaojitokeza ghafla kuwa wenye akili na uwezo mkubwa, na kadhalika.

Yule anayeshindwa, hali yake ni mbaya sana, kwani kushinda si kupoteza uchaguzi tu na fursa ya kutoa mchango katika kuisaidia jamii kuendelea; ni zaidi ya hilo. Kwanza aliyeshindwa huonekana kama mkorofi, kwa sababu tu alithubutu kushindana na yule aliyeshinda.

Namna gani yule anayekuja kushindwa anaweza kujua nani atashinda tangu mwanzo ili asimpinge akaonekana mkorofi baada ya kuwa ameshindwa? Hili ni swali gumu, lakini mantiki ya siasa za Waafrika ni kwamba aliyeshindwa ndiye mkorofi, ndiye mwenye uchu wa madaraka, ndiye anayewagawa wananchi na ndiye mwenye kutaka kuleta vurugu nchini. Hiyo ndiyo mantiki iliyopinda ya Waafrika wengi walio madarakani.

Lakini ukorofi wa yule ambaye hatimaye atashindwa hudhihirika pale ambapo huyo mshindani mkorofi anapompinga aliye madarakani, ndiyo kusema yupo mtawala madarakani, na anaendesha serikali yake vizuri tu, naye anaamini kwamba kazi yake anaifanya kama anavyotakiwa, halafu anajitokeza mtu mwingine kusema anataka jukumu la kuongoza nchi akabidhiwe yeye.

Katika mantiki ya siasa za Kiafrika, ni dhahiri kwamba huyu anayeibuka kusema anataka kumwondoa mtu aliye madarakani ndiye mkorofi, kwa sababu kazi anyoitaka ina mtu tayari, na mtu huyo anaifanya vizuri tu. Haionekani sababu ya mtu mwingine kutaka kuchukua kazi ambayo tayari ina mtu na mtu anaifanya vizuri isipokuwa mkorofi tu.

Kabla hajashindwa mkorofi huyo atafanyiwa kila aina ya vituko ili kumsaidia kuelewa kwamba anachojaribu kukifanya hakiingiii akilini. Atafuatwafuatwa na mawakala wa vyombo vya dola; atasongwasongwa ili asijisikie huru na mwenye nafasi ya kutenda; atapelekewa maneno ya kumtisha na kumkatisha tamaa; atachunguzwa na asasi zinazohusika na kodi au jinai; atadodoswa kuhusu maisha yake binafsi; atachokonolewa kama vile ni nyoka na watu wanataka kuona miguu yake....

Kila juhudi zitafanywa ili kumzuia na labda kumfanya aache dhamira yake ya kutaka kuchukua kazi ambayo tayari inayo mtu na mtu huyo anaifanya vizuri. Baada ya vitisho na kila aina ya hekaheka na uchaguzi ukafanyika, huyo mkorofi akishinda wale walio madarakani wanaweza wakaukataa ushindi huo, wakaufuta. Wanaweza kufanya hivyo kwa sababu uwezo wanao, majeshi wanayo na asasi za utawala zote wanazo.

Imetokea mara kadhaa katika nchi za Kiafrika kwamba wananchi wanapiga kura kumchagua mtu fulani au chama fulani, lakini waliomo madarakani wanakataa, tena kwa nyuso kavu kabisa, kuachia madaraka.

Katika nchi kama hizo, wale waliopigiwa kura na wananchi lakini wakapokonywa ushindi ndio wanaoonekana kama wakorofi, hasa kama wananchi waliokasirishwa na udhalimu wataasi. Waliobiwa ndio wanakuwa watuhumiwa wakuu, na watuhumu wao ni wale waliowaibia.

Sitaki kusema kwamba kila mara walioshindwa wanakuwa wameibiwa, la hasha. Hutokea kwamba walioshindwa wameshindwa kweli, lakini zahama wanazozipata bado ni zile zinazoashiria kwamba ni wakorofi na wavurugaji kwa sababu tu walidiriki kutaka kuchukua nafasi isiyokuwa yao. Watapatilizwa kwa kosa hilo ambalo limeruhusiwa na katiba ya nchi.

Haya si ya kutunga, haya si ya kuzua, mifano tunayo tele. Ukweli ni kwamba Waafrika wengi bado hawajakubali msingi wa siasa za ushindani, bado. Bado tuko katika enzi za ‘mwenye nguvu mpishe’ na hapa nguvu ina maana nguvu za mabavu ya vyombo vya dola, au nguvu za mabavu mbadala, kwani wale wanaohisi wameonewa wanaweza pia kujenga uwezo wao wa kimabavu.

Kwa jinsi hii Waafrika tunajidumaza, hatuendi ko kote. Haishangazi, basi, kwamba baada ya nusu karne ya Uhuru na utawala wetu wenyewe, umasikini unazidi kukua, adha zinazidi kutuandama na ghadhabu za wananchi zinazidi kupanda. Sijui kama watawala wetu wanaliona hilo, na kama wanaliona sijui kama wanaamini kwamba njia ya kukabiliana nalo ni kutoa matamshi ya kutishana.

Matamko ya hivi karibuni kutoka kwa vyombo vilivyo karibu mno na utawala yanatia shaka kwamba watawala wanataka kuwafanya wananchi waamini kwamba wale wanaowapinga ni wakorofi na wachokozi. Inatia hofu kwamba labda na sisi hatujaondokana na mantiki niliyoieleza hapo juu. Matamko haya hayafai kwa sababu ni ya hatari.

Tunahitaji kufanya hadhari kubwa ili kuepusha janga kuu.

Wednesday 6 October 2010

Mficha uchi hazai

Mimi naitwa jina langu Sijali nimelelewa na nyanya wangu nikiwa mdogo na kwa babati nzuri nikasoma elimu chekechea katika kituo cha wazungu. Sasa raha na tabu ya umombo na mchanganyiko wa lugha za kigeni kutoka ulaya zilinisababisha kuwa na wakati mgumu sana pale gharama ya kusoma shule pamoja wazungu ilipokuwa kubwa kuliko uwezo wa kifedha kumudu gharama ya ada kutoka kwa nyanya wangu. Basi nikalazimika kujiunga na darasa la kwanza kwenye shule zetu za serikali.

Lugha rasmi katika shule za msingi hapa Tanzania kama inavyofahamika ni Kiswahili tangu darasa la kwanza mpaka kufikia darasa la saba. Ingawa kwa wakati huo lugha ya kiengereza ilitumika kama somo utakapofikia darasa tatu. Sasa hali ilikuwa ngumu kweli kwa upande wangu katika kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili, ingawa kuongea haikuwa shida.

Somo la hisabati kwa sababu lenyewe sehemu kubwa ya shughuli zake za kiada zinategemea tarakimu na pia kama lugha moja duniani. Hivyo haikuwa na shala isipokuwa tuu. Iwapo swali kama linatakuwa limeandikwa ama kutungwa kwa maneno ya Kiswahili basi hali iliendelea kuwa mbaya.

Kimsingi nilikuwa sijishughulishi kabisa na hali hiyo maswali yanayokuwa na maelezo tena hasa ya Kiswahili, nikitegemea kwamba iwapo sitajibu basi yale maswali hisabati yenye tarakimu ambayo nilikuwa mzuri sana kwenye hilo yatanilinda kupata alama. Kitu cha kusikitisha masomo mengine yote yaliobaki yalikuwa na sifa(kusoma na kuandika,) ambazo mimi sikuwanazo.

Sasa kwa sababu za bora liende la mwalimu wetu wa darasa la kwanza, na wakati huo ilikuwa mwalimu anayeanza wanafunzi darasa la kwanza alikuwa akiendelea na wanafunzi kuingia darasa la pili. Hivyo mimi niliendela na ubovu wangu huo bila ya kupata usaidizi wa karibu wa kutoka mwalimu na mimi kama mwanafunzi nisiye fahamu kwamba hicho nachofanya kitaniletea madhara maishani.

Nikawa naona ni unafuu na ujanja kumtoroka mwalimu na kuishi kama mwanafunzi ambaye hawezi kusoma ama kuandika.Sasa hapo nyumbani nilipokuwa naishi ndipo palipoweza kugundulika udhaifu wangu maana huyo nyanya yeye kitaaluma alikuwa ni Mwalimu.

Siku moja akaniomba ripoti ya kimasomo yangu ya jumla ya mwaka ya darasa la pili wakati huo tulikuwa tunakabidhiwa wanafunzi na kuleta nyumbani . Mimi nilikuwa na ujanja wa kubadirisha tarakimu.

Hivyo nilijichanganya zile sehemu ambazo unatakiwa ujue kusoma na kuandika lugha kiswahili ili kuweza kurekebisha. Sasa sehemu inayojaza na nafasi ya mwanafunzi darasani kwenye tarakimu ilionyesha nipo nafasi ya kumi na nane kati ya wanafunzi mia moja, Ingawa ukweli wenyewe nilikuwa na nafasi ya tisini na nane.

Na hiyo ndiyo maneno yalikuwa yameandikwa kwa lguha ya Kiswahili. Basi nyanya yangu akashtukia kitu pale.Akasema naomba kachukue kile kitabu cha darasa kwanza cha Juma na Roza, Nategemea kila mtu aliyesoma wakti huo anakifahamu vizuri. Akafungua ukurasa mmoja nisome. Nilipoona tuu picha nikakumbuka ile hadithi niliyosomewa na baadhi marafiki zangu niliyokunasoma nao. Nikaaanza kusoma kwa jinsi nilivyokariri. Maana suala ilo nilikuwa mzuri na hodari sana wakukariri.

Nyanya yangu aukupata kitu hapo ingawa bado taaluma yake ilikuwa inamwambia kuwa kuna kitu kinaendelea upande, baada ya kuona mkorogo kwenye taarifa yangu ya mwaka ya kimasomo. Sasa tatizo kubwa ilikuwa wakati huo shule zimefunga hivyo hawezi kufuatilia mpaka ya mwezi na nitakuwa naingia darasa la tatu.

Kutokana na hali basi alihamua kunikabidhi kwa mwalimu mwenzake ambaye anasifikia kwa kufundisha vizuri na kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi. Basi ya baada kufungua shule niliambiwa na Nyanya yangu kwamba nalazimika kukaa na huyo mwalimu kwenye darasa kwa muda wa juma moja kabla sijaendelea na darasa la tatu.

Kwa kuanzia tuu yule mwalimu alikuwa hatumii kitabu katika kusoma ama kuandika. Hivyo hadithi yeyote iliyopo kitabuni inaandikwa ubaoni tena bila picha. Sasa hapo na mimi nilikuwa nimepangiwa nikahe kiti cha kwanza kabisa, na pia nilichaguliwa kuwa mtu wa kwanza kusoma kwa siku hiyo, tena unatumia fimbo kuonesha maneno unayosoma, neon moja baada la jingine.

Na hapo ndiyo siri yangu ilipofichuka tena darasa lote wakijua kwamba siwezi kusoma na kuandika Kiswahili. Na pia hiyo taarifa ikawa imemfikia Nyanya wangu. Na hiyo ndiyo ilikuwa tiketi ya kubaki lile darasa la pili badala ya kuendelea darasa la tatu.

Nakubali na pia naamini yule mwalimu aliyetumia ujanja wa kujua siri yangu na nyanya wangu hawa wote walikuwa wananitakia mema maishani mwangu. Maana huyo mwalimua na huyo nyanya wote wamefariki hivi sasa wakati naandika hii habari kwa kifupi kuhusu maisha yangu huko nyuma.

Kimsingi nataka kuzungumzia siasa za hapa nyumabani Tanzania kwamba wananchi waache kuchagua viongozi kwa mazoea maana hayawezi kukusaidia kwa mikakati ya muda mrefu. Iwapo unahitaji maendeleo tusiendelee mpaka watokee malaika kama hawa walionisaidia mimi leo kuweza kujua kusoma, kuandika Kiswahili.

Kupiga kura kwa kiongozi kwa sababu mazoea utaishia kuwa kama mimi nilivyokuwa katika elimu ya awali mzuri wa tarakimu tuu na siyo maandishi anayepata hasara hapo ilikuwa ni mimi, Wakti mwalimu yeye alikuwa akiendelea kulipwa mshahara wake. pamoja kuwa nilikuwa sipati maarifa yoyote kutoka kwa yule mwalimu wa kwanza. Hivyo unapochagua viongozi wabovu pia inapelekea kuwa na maamuzi mabovu.

Siasa ni muhimili wa nchi kwa kila jambo, tusichagua wabunge, madiwani na hta pia rais kwa ajili ya mazoea. Iwapo kama tunataka na pia tunahitaji maendeleo basi hilo halina mjadala kiongozi anatakiwa awe shupavu wa utendaji anafuata misingi na sheria zilizopo na siyo maneno na ubabaishaji.

Ambayo kimsingi kama ni Rais, au mmbunge ataendelea kupokea mshahara na posho. Wakati huo huo sisi wapiga kura tukiendelea kuwa maisha shida na dhiki isiyokuwa na kipimo.

Inaendeleo siku zijazo hizi zitakuwa makala mfululizo kadri navyopata muda wa kuandika